Tangaza na Abd Da Hustler

1. TAARIFA KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA DENGUE “DENGUE FEVER” 2.


 
Utangulizi

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “ dengue fever” hapa nchini. Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa wagonjwa waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu kepelekwa kwenye maabara ya NIMR, Dar es salaam na kuthibitisha kuwa na virusi vya “dengue fever” mnamo tarehe Juni 9, 2010 .
Hadi sasa Idadi ya wagonjwa ambao wameripotiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu ni 37 na hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha. Kati ya wagonjwa hao wagonjwa 24 wamethibitishwa kuwa na virusi vya Dengue fever, watatu kati yao ni watanzania


 
Homa ya Dengue

Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kiitwacho dengue virus ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes. Jamii ya Mbu huyu ndiye pia hueneza ugonjwa wa homa ya manjano yaani “ yellow fever” . Dalili za ugonjwa huu ni homa ya ghafla,mwili kuchoka, kuumwa na viungo, kuvimba tezi na kupatwa na harara (rashes). Uwepo wa homa, harara (rash) na kuumwa kichwa ndio dalili kuu 3 kuu za ugonjwa huu. Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na14 (kwa kawaida ni siku 4-7). Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za ugonjwa wa malaria,hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa macho haswa wakati wakipata homa ambazo zinafanana na malaria lakini wakipimwa malaria inakuwa haionekani.

Kuna aina 3 tofauti za ugonjwa huu kama zifuatazo;

• i. .Dengue Fever : Aina hii ya homa ya dengue huambatana na dalili kuu tatu za homa kali ya ghafla, harara (rash) na kuumwa kichwa

• ii. Dengue Hemorrhagic Fever : Aina hii ya homa ya dengue huambatana na dalili za mgonjwa kutokwa na damu kwenye fizi au puani,vile vile kutokwa na damu chini ya ngozi (Petechial Haemmorhage) na iwapo mgonjwa huyu ataumia sehemu yoyote ni rahisi kwake kupoteza damu nyingi kupitia kwenye michubuko

• iii. Dengue Shock syndrome : Aina hii ya homa ya dengue huambatana na mgonjwa kupoteza damu nyingi ambayo hupelekea kupata shock na mgonjwa anaweza kupoteza fahamu.
Aina ya pili na ya tatu ni aina zenye dalili mbaya ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa na hatimaye kupelekea mgonjwa kufariki. Mpaka sasa hapa Tanzania tumepata wagonjwa wenye dalili ya kwanza yaani dengue fever
 
 

Homa ya Dengue inavyoambukiza 

Virusi vya homa ya dengue vinaenezwa kwa binadamu baada ya kuumwa na mbu aina ya “ Aedes ” .Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Inasadikika kuwa viwavi wa mbu hawa huweza kuishi katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu.

 

 
 
Je ugonjwa huu unaweza kuambukizwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu?
Hapana. Ugonjwa huu hauenezwi kutoka binadamu mmoja kwenda kwa mwingine bali ugonjwa huu huenezwa na mbu aliyeambukizwa na virusi vya homa ya dengue anapomuuma binadamu..
Je,ugonjwa huu unatibika?
Ndio,Ugonjwa wa homa ya dengue unaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka.Hakuna tiba maalumu ya ugonjwa huu bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu vile vile hadi sasa hakuna chanjo kwa ajili ya kinga kwa binadamu.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
•  Kuangamiza mazalio ya mbu
•  Fukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua vimelea vya mbu kwenye madimbwi hayo
•  Ondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi,makopo nk.
•  Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
•  Funika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara
•  Kujikinga na kuumwa na mbu
•  Tumia dawa za kufukuza mbu“mosquito repellants”
•  Vaa nguo ndefu
•  Tumia vyandarua vilivyotibiwa
•  Weka wavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Afya na ustawi wa jamii
Kutoa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa katika ofisi za Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar
•  Watumishi wa afya wa wilaya zote 3 za Dar es salaam wamepewa mafunzo ya ziada ya namna ya kutambua,kutibu na kuthibitisha ugonjwa huu
•  Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika hospitali 3 za wilaya za Dar es salaam na hospitali ya Mnazi mmoja Zanzibar
Kuimarisha Utambuzi wa ugonjwa katika maabara ya NIMR, Dar es salaam
•  Wizara imeshapatiwa msaada na CDC wa vitendanishi(Primers na Probes) ili kuweza kuthibitisha ugonjwa huu
Kuimarisha Uwepo wa ugonjwa huu katika mbu
Wizara kwa kushirikiana na NIMR itafanya utafiti wa kuwepo kwa virusi vya ugonjwa huu katika mbu aina ya Aedes Aegypt
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyekwisha kufariki. Vile vile wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
 

Share on Google Plus

About Unknown

Naitwa Abdalla Ngowi, Napenda Michezo na kukupa habari mbalimbali kutoka katika kila kona ya ulimwengu huu!, karibu ABD da Hustler
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 MAONI :

Post a Comment