Tangaza na Abd Da Hustler

ZITTO"DENI LA TAIFA WANAFAIDI WEZI WACHACHE LAKINI TUNALIPA WOTE"

Deni la Taifa: wafaidi wachache, twalipa wote.
Leo nimeandika kuhusu Deni la Taifa kukua kwa kasi na kufikia tshs 27 trilioni mpaka Desemba 2013 kutoka tshs 10 trilioni mwaka 2005. Baadhi ya Watalaamu wanajenga hoja kuwa kukopa sio shida, bali kukopa kwa ajili ya nini. Nikakumbuka mzigo wa madeni ambao Taifa lilibeba miaka ya sabini na themanini kiasi cha Tanzania kukoswa koswa kuwa nchi ya Kwanza duniani kushindwa kuhudumia madeni yake. ‘heshima’ hiyo ilikwenda kwa nchi ya Nicaragua mwaka 1982. Mikopo ya nini?
Mwishoni mwa miaka ya sabini Tanzania ilikopa dola za kimarekani milioni sitini (USD 60m) kwa ajili ya mradi wa Kiwanda cha viatu Morogoro. Lengo la kiwanda kiwanda kile ilikuwa ni kuuza viatu nchini Italia. Mwaka mmoja baada ya kiwanda kuzinduliwa kilikuwa na uwezo wa kuzalisha kwa ufanisi wa asilimia 4 tu ya uwezo wake na hakikuweza kuuza hata jozi moja ya kiatu nje ya nchi. Miaka ya tisini kiwanda kile kiliuzwa katika mpango wa ubinafsishaji na hivi sasa kimegeuzwa kuwa ghala. Hata hivyo Deni hili lilipwa na kila Mtanzania kupitia kodi.
Kesho Jumanne tarehe 28 Januari, 2014 Kamati ya Bunge ninayoongoza ya Hesabu za Serikali (PAC) inapokea taarifa ya ukaguzi maalumu uliofanywa kuhusu Mfumo na Mchakato wa kusambaza pembejeo za ruzuku kwa wakulima. Ukaguzi huu umefanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG). Nimeipitia Taarifa hii na kukumbuka habari ya ‘Morogoro Shoe Factory’.
Bajeti ya pembejeo za ruzuku ya mwaka 2011/12 ilikuwa tshs 122.4 bilioni, kati ya hizo tshs 88.9 bilioni ni mkopo kutoka Benki ya Dunia. Taarifa ya CAG inaonyesha uvundo wa ufisadi katika mfumo mzima wa pembejeo za ruzuku. Katika kijiji cha Lunyala wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa asilimia 70 ya wananchi waliorodheshwa kupata mbolea walikuwa bandia, hata hao waliopata mbolea walidai mbolea ilikuwa haina ubora stahili na matokeo yake uzalishaji wa mazao ulikuwa mdogo. Hata hivyo wasambaji wa mbolea walilipwa fedha zao zote. Afisa mmoja mwandamizi wa Benki ya Dunia alipata nukuliwa kusema kuwa asilimia 60 ya Bajeti ya pembejeo za ruzuku iliporwa na wajanja wachache. 
Deni hili nalo litalipwa na Watanzania wote japo waliofadika ni wezi wachache. Kinachosikitisha ni kwamba masuala haya yanayohusu wananchi hayapati msukumo kwenye mijadala ya kitaifa. Tusipobadilika tutajikuta tuna madeni mpaka kwenye kope za macho yetu. 
“...mikopo haisaidii, hata tukiitumia kujenga shule au hospitali au viwanda lazima ilipwe. Mlipaji ni mkulima wa vijijini...” Azimio la Arusha, 1967.
Share on Google Plus

About Unknown

Naitwa Abdalla Ngowi, Napenda Michezo na kukupa habari mbalimbali kutoka katika kila kona ya ulimwengu huu!, karibu ABD da Hustler
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 MAONI :

Post a Comment