![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgA3I7E3AdvfUonRM73SLWZ8fUng3oUKxhFFed4FcQXhe6jyByiayrYAJxTbFnDfAAeNY_roAU2PrC6FRveXNZyVZscGElPOyNi0nU4w3MWgBtDxcmcLW5BwdoqlvEzu-vSU0Gi2-n5uHY/s1600/okwi.jpg%3Fw=506.jpeg)
Na BARAKA MBOLEMBOLE
Wakati ligi kuu ikianza, mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi, Mganda, Emmanuel Okwi amekuwa mmoja wa watazamaji mwenye thamani kubwa. Je, Yanga wameingia ' mkenge' katika usajili wake?. Hili linaweza kuwa swali ambalo majibu yake yapo wazi. Kwanza, Okwi ni mchezaji wa Etoile du Salehe ya Tunisia ambao walimnunua kutoka timu ya Simba.Kwa nini yupo Yanga?. Alikuwa akiichezea timu ya SC Villa ya kwao Uganda kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita akitokea Etoile. Narudia tena, alikuwa akiichezea Villa kwa mkopo. Fifa ilimruhusu Okwi kucheza Villa kwa muda wakati kesi tatu zinazomuhusu Mganda huyo zikitafutiwa mhuafaka. Okwi kwa upande wake anadai kuwa Watunisia hao walivunja mkataba kwa kushindwa kumlipa pesa zake kama ilivyotakiwa. Simba nao wanadai malipo yao kutoka kwa Etoile.
Okwi
aliruhusiwa kuichezea Villa ili kulinda kiwango chake, na wala hakuwa
mchezaji anayemilikiwa na timu hiyo. Alizuiwa kuichezea timu ya Taifa ya
Uganda katika michuano inayoendelea ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji
wa ligi za ndani, CHAN, kwa kuwa alikuwa Villa kwa mkopo kutoka timu ya
ng'ambo. Ila, ni Villa ndiyo wanaosemekana kumuuza Okwi kwa timu ya
Yanga. Kwa mamlaka gani?. Hadi hapa Yanga watakuwa wameliwa. Kwa kuwa
Okwi ni mchezaji wa Etoile si Villa.
Yanga
wamemsaini Okwi huku wakijiaminisha kuwa wapo sahihi. Wanaamini Okwi ni
mchezaji huru au wa Villa. Ila, alitakiwa kucheza Villa kwa miezi sita,
lakini akaitumikia miezi isiyozidi miwili tu na kununuliwa. Caf,
Shirikisho la soka Afrika wamemuhidhinisha Okwi kuichezea Yanga. Kamati
ya sheria na hadhi ya wachezaji imemzuia matumizi yake hadi watakapopata
ufafanuzi kutoka FIFA, Shirikisho la soka ulimwenguni.
Ndiyo, wapo sahihi kwa kuwa FIFA, ndiyo waliosema mchezaji huyo acheze Villa kwa miezi sita wakati kesi zake zikishughulikiwa.
FIFA, wanaweza
kumruhusu Okwi kuchezea Yanga kwa maslai ya kipaji chake. Ila, wanaweza
pia kumzuia endapo watajua kuwa mchezaji huyu amekiuka maagizo yao ya
awali ambayo walimwambia acheze Villa. Inawezekana mchezaji huyo
akaonekana tapeli, kwa kuwaadaa Yanga wakati akijua fika mkataba wake
upo Etoile. Wapo wachezaji walioshinda vita kama hii ya Okwi, ila wapo
pia walioingia katika vifungo vya FIFA.
Huenda Yanga
wakamtumia Okwi siku za mbele, ila kwa sasa ni uhalali wa mchezaji huyo.
Kama, Etoile wataendelea kushikilia msimamo wao kuwa hawajui mchezaji
wao mahali alipo, Okwi ataoneka ni mtoro. Endapo, Okwi ataonekana ni
halali madai yake anaweza kulipwa fidia na Etoile, ila kasheshe ni wapi
ambapo Villa walipata kibali cha kumuuza Okwi kwa timu ya Yanga?
Kila upande
udai una wanasheria wake. Duh!. Lakini mwanasheria wa Okwi anaweza kuwa
mjanja zaidi, mwenye akili zaidi, kwa kuweza kupata saini na mamillioni
ya Yanga kwa ufafanuzi wake wakati akimpigia debe mteja wake kuwa hana
tatizo. Kama sheria iliwekwa ili ivunjwe, na kama mikataba siku zote
inaweza kutenguliwa, Yanga watamtumia Okwi, ila tusije kushangaa FIFA,
wakisema mchezaji huyo mali ya Etoile. Yanga walimnunua wapi Emmanuel
Okwi? Labda hapa ndipo kuna hoja ya msingi.
0714 08 43 08
0 MAONI :
Post a Comment