Katika siku za hivi karibuni, Kapombe alidaiwa kuwaniwa na Yanga na
Azam FC ili asajiliwe kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na tayari timu
zilishafanya naye mazungumzo ya siri.
Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili
ya Simba, Zacharia Hanspope alisema, Cannes wanaoshikilia haki za
Kapombe, wamefikia uamuzi wa kutaka kumuuza beki huyo baada ya kushindwa
kuvumilia usumbufu wa mchezaji huyo ambaye hadi sasa bado yupo nchini.
Hanspope alisema, Cannes imewaagiza Simba kulipa gharama
walizozitumia katika kumtibu na kuimarisha kiwango cha nyota huyo kwa
muda alioishi nchini Ufaransa. Gharama hizo ni Euro 33,000 ambazo ni
zaidi ya Sh. 73.1 milioni.
Bosi huyo mwenye nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya Simba ambaye kundi
la Friends of Simba linataka kumpendekeza kuwania Uenyekiti wa klabu
kwenye uchaguzi wa Mei 4, alisema klabu yake imekubali kulipa gharama
hizo kwa lengo la kuokoa kipaji cha Kapombe baada ya kubaini mpango wa
moja ya klabu za hapa kutaka kumsajili. Kapombe amefungua kesi
Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa) baada ya Cannes kushindwa kumlipa
mshahara wake wa miezi mitatu.
“Simba tupo tayari kumrudisha Kapombe, tumeshazungumza na Cannes
wamesema wanataka kurudishiwa gharama zao, pia wapo tayari kushusha
zaidi, ndiyo tunasubiri watuambie wanachotaka kutupunguzia ili nasi
tujipange kuwalipa, hata mchezaji mwenyewe hana shida katika kurudi
hapa,” alisema Hanspope.
Kufuatia taarifa hizo, Mwanaspoti lilimtafuta meneja wa Kapombe
ambaye pia ni wakala wake, Denis Kadito anayeishi Uholanzi ambaye
alisema anafanya mazungumzo na taasisi kadhaa ili kuokoa kipaji cha
mchezaji huyo lakini hakukiri kwamba ni Simba wala hakutaka kufafanua.
“Siwezi kuzungumzia suala la Kapombe kwa sasa, sababu kubwa moja ni
kwamba nipo katika mazungumzo na Cannes na taasisi nyingine ili kuokoa
kipaji cha mchezaji, naomba mnipe wiki moja nitakuwa katika nafasi nzuri
ya kuzungumzia hilo,” alisema Kadito.
Aidha Kapombe mwenyewe alipotafutwa alisema:”Sitaki kuzungumzia suala
lolote kuhusiana na mpira kwa sasa, kama kuna taarifa zozote umezipata
kutoka sehemu nyingine ndiyo hivyo hivyo.”
0 MAONI :
Post a Comment