Msemaji wa Wizara ya Nje ya Marekani, Jen Psaki, amesema mkutano huo wa mjini Washington unaweka msingi wa mwanzo wa mazungumzo, akiongeza kwamba pande zinazohusika zitaandaa ratiba ya namna ambavyo hatua za mazungumzo zitapigwa kwenye miezi ijayo.
Waziri wa Sheria wa Isreal ambaye ndiye kiongozi wa nchi hiyo kwenye mazungumzo ya amani na Palestina, Tzipi Livni, akiwa pamoja na msaidizi wake wa masuala ya kisheria, Yitzhak Molcho, watakutana kwanza na kiongozi wa ujumbe wa Palestina, Saeb Erakat, anayeambatana na afisa wa ngazi za juu katika serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mohammed Shtayyeh, katika futari iliyoandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, jijini Washington, jioni ya leo.
Msemaji wa Wizara ya Nje ya Marekani, amesema mikutano ya awali imepangwa kufanyika leo na kesho, Jumanne, huku Kerry akisema viongozi wote wawili wameonesha utayarifu wa kuchukua maamuzi magumu, na amewashukuru kwa kujitolea kwao.
Kuachiwa kwa wafungwa wa Kipalestina
Baadhi ya waandamanaji mjini Jerusalem wakipinga kuachiwa huru kwa wafungwa wa Kipalestina.
Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, alikutana na baraza lake la mawaziri akipigania kuwashawishi baadhi ya washirika wa serikali yake ya mseto kukubaliana na hatua hiyo na ile ya kurejea kwenye mazungumzo na Wapalestina.
"Naamini kurudi kwenye mchakato wa kidiplomasia katika wakati huu ni muhimu kwa taifa la Israel, kwa sababu ya kujaribu kuumaliza kabisa mgogoro huu mrefu na pia kutokana na hali ilivyo kwenye eneo letu, kama inavyooneshwa na changamoto za usalama za Syria na Iran. Makubaliano yoyote yatakayofikiwa kwenye mazungumzo hayo, yatapigiwa kura ya maoni." Aliahidi Netanyahu.
Netanyahu apingwa
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Palestina.
Licha ya ahadi hiyo, hatimaye baraza hilo lilipitisha kuachiwa
kwa wafungwa kwa kura 12 tu kati ya wajumbe 22, huku saba zikipinga na
wawili wakijiepusha kupiga kura zao.Naibu Waziri wa Ulinzi anayetokea chama chenye itikadi kali cha Likud, Danny Danon, aliongoza kampeni ya kupinga mpango huo, akisema ni makosa ya kidiplomasia na ya kimaadili.
"Napingana na uamuzi huu. Nadhani Israel hairuhusiwi kuwaachia huru magaidi hao waliowaua Mayahudi. Na nadhani tunaweza kuzungumza na Wapalestina bila ya mambo hayo ya kutisha." Alisema Danon.
Kiongozi wa ujumbe wa Palestina kwenye mazungumzo hayo aliikaribisha kura iliyopigwa na baraza la mawaziri la Israel, akiita hatua muhimu. "Natarajia tutaweza sote kuitumia vyema fursa hii iliyoletwa na juhudi za uongozi wa Marekani", aliliambia shirika la habari la AFP.
Awamu ya mwisho ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Israel na Palestina, yaliyoengwaenga na Rais Barack Obama, ilivunjika mwaka 2010 kutokana na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.
0 MAONI :
Post a Comment