Rais wa Bolivia, Evo Morales ametishia kuufunga ubalozi wa Marekani
nchini Bolivia kutokana na kiongozi huyo kudai kuwa nchi hiyo ilihusika
kuizuia ndege yake kupita kwenye anga ya nchi kadhaa za Ulaya.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kushuku kwamba Edward Snowden,
aliyevujisha taarifa za siri za kijasusi za Marekani, yumo ndani ya
ndege hiyo. Akizungumza katika mji wa Cochabamba nchini Bolivia, Rais
Morales ameituhumu Marekani kwa kuyashinikiza mataifa kadhaa ya Ulaya
kuzuia anga zao na kutoiruhusu ndege yake kupita.Amesema Bolivia iko huru na ina hadhi yake, na kwamba hata bila Marekani, nchi hiyo itasimama imara kisiasa na kidemokrasia, hivyo hawauhitaji ubalozi wa Marekani. Rais Morales aliwasili nchini kwake Jumatano iliyopita, akitokea Vienna, Austria, baada ya ndege yake kuzuiwa kupita kwenye anga ya mataifa manne ya Ulaya na kulazimishwa kwenda Austria.
Viongozi wa Amerika ya Kusini wakutana
Kufuatia hatua hiyo, viongozi wa mataifa ya Amerika ya Kusini walikutana mjini Cochabamba kuzungumzia tukio hilo. Katika mkutano huo wa dharura na Rais Morales, marais wa Venezuela, Argentina, Ecuador, Uruguay na Surinam, wamezitaka nchi za Ulaya zilizohusika ambazo ni Uhispania, Ufaransa, Italia na Ureno, kuomba radhi kutokana na kitendo hicho walichokifanya. Viongozi hao wamesema kuwa kitendo hicho ni tusi kwa Bolivia na Amerika ya Kusini kwa ujumla, ambayo imeshuhudia mapinduzi kadhaa ya kijeshi yaliyoungwa mkono na Marekani.
Hata hivyo, Waziri wa masuala ya kigeni wa Uhispania, Jose Manuel Garcia-Margallo, amesema nchi yake haikumzuia Morales kutua kwenye ardhi yake. Viongozi hao wa Amerika ya Kusini wamesema kwa pamoja wataendelea kupambana dhidi ya ubeberu unaofanywa na Marekani. Serikali ya Morales imekuwa katika uhusiano usio mzuri na Marekeni, ambapo mwaka 2008 Bolivia ilimfukuza balozi wa Marekani nchini humo pamoja na maafisa wa shirika la kupambana na madawa ya kulevya la Marekani kutokana na hatua yao ya kuwachochea wapinzani. Hadi sasa, serikali ya Marekani imekataa kuzungumzia iwapo ilihusika katika hatua ya kuzuia anga ya nchi hizo za Ulaya.
0 MAONI :
Post a Comment