![candidiasis](http://4.bp.blogspot.com/-Jwe2sPTng9o/T2YnjtUJtgI/AAAAAAAAG7c/PjKx8GCzp7Q/s320/CANDIDIASIS.jpg)
Kati
ya maambukizi yanayowasumbua wanawake wengi duniani ni maambukizi ya
fangasi. Inakisiwa asilimia 75 ya wanawake wote duniani hupata
maambukizi haya katika kipindi cha uhai wao.
Maambukizi ya fangasi katika sehemu za siri za mwanamke husababishwa na uwepo wa fangasi wanaojulikana kitaalamu kama Candida albicans.
Maambukizi haya pia hujulikana kama yeast infection au thrush. Fangasi
hupatikana kama vimelea vya kawaida katika mdomo, mpira wa kupitisha
chakula sehemu inayojulikana kama pharynx, katika kibofu cha mkojo, uume na hata kwenye uke.
Mfumo
mzuri wa kinga wa mwili pamoja aina fulani za bakteria wanaoishi
pamoja na fangasi hawa husaidia sana katika kuthibiti maambukizi
yanayoyosababishwa na aina hi ya fangasi.
Nini hutokea?
Kwa kawaida, Candida albicans
huishi kwenye uke na sehemu nyingine (kama zilivyoelezewa hapo juu)
bila kusababisha madhara yoyote yale isipokuwa pale mazingira ya eneo
husika yanapobadilika kama vile mabadiliko katika hali ya pH ya eneo
husika (ifahamike ya kwamba pH ya kawaida ndani ya uke ni 4.0 - 4.5) au
uwiano wake na vimelea (microorganisms) wengine
unapoharibiwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya
madawa aina ya antibiotics, kupungua kwa kinga mwilini kutokana na
magonjwa mbalimbali n.k.
Maambukizi haya ya fangasi yanaweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili;
1.
Maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated thrush: Katika kundi
hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi mara moja hadi nne kwa mwaka na
dalili zake huwa si mbaya sana na maambukizi haya husababishwa na
fangasi wa jamii hii ya Candida albicans.
2.
Maambukizi makali yaani complicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa
hupatwa na maambukizi zaidi ya mara nne kwa mwaka, dalili zake kuwa
mbaya zaidi au kama maambukizi yatakuwa yametokea kipindi cha ujauzito,
ugonjwa wa kisukari, upungufu wa kinga mwilini. Aina hii kusababishwa
na vimelea vya aina nyingine tofauti na Candida albicans.
Vihatarishi
Watu walio katika hatari ya kupata maambukizi ya fangasi hawa ni wale wenye;
•
Kutumia sana dawa aina ya detergents kwenye sehemu za siri au douches
(vifaa vinavyotumiwa kusafishia uke kwa kutumia maji yaliyochanganywa
na siki au antiseptic yoyote ile) kwa sababu hali husababisha
kuharibika kwa uwiano wa fangasi na aina nyingine ya vinyemelezi kama
bakteria aina ya lactobacilli
• Kutumia sana madawa aina ya antibiotics, steroids ambayo yana tabia ya kushusha kinga ya mwili
•
Mabadiliko ya mfumo wa homoni mwilini ambayo husababisha mabadiliko
katika s ehemu za siri na hivyo kufanya kuwepo kwa ukuaji wa kasi wa
fangasi hawa
•
Ujauzito (kutokana na kubadilika kwa mfumo wa homoni mwilini na
kupungua kwa kinga ya mwili). Hata hivyo ieleweke hapa kuwa si kila
mjamzito hupatwa na maambukizi haya.
• Matumizi ya dawa za kupanga uzazi (vidonge vya majira)
•
Upungufu wa kinga mwilini kutokana na magonjwa sugu kama kisukari,
saratani aina yoyote ile, ugonjwa aina ya mononucleosis na nk.
• Ugonjwa wa ukimwi (HIV/AIDS)
• Matibabu ya homoni (hormonal replacement therapy) kutokana na sababu mbalimbali
• Matibabu ya kusaidia kushika mimba kwa wale wenye matatizo ya uzazi (infertility treatment)
• Msongo wa mawazo (stress)
• Utapia mlo (malnutrition)
•
Kuvaa nguo au mavazi yanayoleta joto sana sehemu za siri kwa muda
mrefu kama nguo za kuogelea (swimwear), nguo za ndani (chupi)
zilizotengenezwa kwa kitambaa aina ya nylon, nguo za ndani zinazobana
sana nk.
•
Kujamiana kwa njia ya kawaida mara tu baada ya kujamiana kupitia njia
ya haja kubwa au matumizi ya vilainishi venye glycerin wakati wa
kujamiana pia yamehusishwa na maambukizi haya.
• Kuvimba kwa tezi la koo (goiter)
• Saratani ya tezi la koo (thyroid cancer)
•
Wanawake wenye umri wa miaka kati ya ishirini na thelathini wapo
kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi haya wakati wale ambao
wameshaacha kupata hedhi au wale ambao hawajaanza kupata hedhi kabisa
hawako kwenye hatari kubwa.
Kwa wanaume vihatarishi vya maambukizi haya ni;
• Kujamiana na mwanamke mwenye tatizo hili au maambukizi haya
• Upungufu wa kinga mwilini
• Matumizi ya madawa aina ya antibiotics kwa muda mrefu bila ushauri wa daktari
• Magonjwa sugu kama kisukari, saratani ya aina yoyote ile na nk.
Dalili na viashiria kwa wanawake;
• Kuwashwa sehemu za siri (kwenye tupu ya mwanamke)
• Kuhisi kuwaka moto sehemu za siri (burning sensation)
• Kufanya kama vidonda katika sehemu za siri (soreness)
• Maumivu wakati wa kujamiana (superficial dyspareunia)
• Maumivu au usumbufu wakati wa kujisaidia haja ndogo (wakati mtu anakojoa)
• Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwa mdomo wa nje wa tupu ya mwanamke (labia minora)
• Kutokwa na uchafu wa rangi nyeupe au nyeupe kijivu, unaoweza kuwa mwepesi, majimaji au mzito na ambao umefanana na jibini (cottage cheese like discharge) wenye muonekano unaojulikana pia kama curd-like appearance. Kwa kawaida, uchafu huu haumbatani na harufu yoyote isipokuwa panapokuwa na tatizo la ziada kama ugonjwa wa zinaa aina ya Bacteria vaginosis. Uchafu huu unaotoka hapa unaweza kuenea kwenye maeneo mengine yaliyokaribu na tupu ya mwanamke kama kwenye mitoki (groin area) au perineum na kusababisha kuharibika kwa ngozi katika sehemu hizo.
Dalili na viashiria hivi huwa mbaya zaidi wakati mwanamke anapokaribia kupata hedhi.
Dalili na viashiria kwa wanaume ni;
• Kuwashwa sehemu za siri
• Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwenye ncha ya uume
• Kuwepo kwa uchafu wa rangi nyeupe (kama nilivyoeleza hapo juu) kwenye sehemu ya juu ya uume.
• Kuwa na vidonda vidogo kwenye uume (sore on the glans)
Hata
hivyo, mara nyingi wanaume hawaoneshi dalili zozote zile, ni vizuri
kwa mwanamke kumueleza mwenza wake pale anapopata maambukizi haya ili
naye pia apate kutibiwa.
Vipimo vya uchunguzi
Kabla ya vipimo vya uchunguzi, ni muhimu kwa daktari kuchukua historia ya mgonjwa kwa usahihi kabisa. Vipimo vitahusisha;
1. Uchunguzi wa uke (
(PV exam) – Daktari huvaa gloves, na kuzilainisha gloves hizi kwa jelly maalum, mgonjwa hulala kwenye kitanda na kutanua miguu yake ili njia itanuke na kumrahisishia daktari kumfanyia uchunguzi, wakati akiwa tayari, daktari ataingiza vidole vyake viwili (cha shahada na cha kati) ukeni kwa dhumuni la
(PV exam) – Daktari huvaa gloves, na kuzilainisha gloves hizi kwa jelly maalum, mgonjwa hulala kwenye kitanda na kutanua miguu yake ili njia itanuke na kumrahisishia daktari kumfanyia uchunguzi, wakati akiwa tayari, daktari ataingiza vidole vyake viwili (cha shahada na cha kati) ukeni kwa dhumuni la
i. Kuhisi kama kuna uvimbe wowote ndani ya tupu ya mwanamke
ii. Kuangalia kama anapata maumivu wakati wa kujamiana
iii. Kuangalia kama kuna uchafu wowote unaotoka, wingi wake, rangi
yake, harufu yake, uzito wake (mwepesi, majimaji au mzito), na aina ya
uchafu unaotoka kama ni sahihi kutokana na maelezo ya mgonjwa au ni
tofauti
iv. Kuangalia kama sehemu ya siri ipo kawaida
v. Kuangalia kama kuna uvimbe wowote wa tezi za sehemu ya siri (mitoki)
vi. Kuangalia nywele za sehemu za siri zilivyo na jinsi zilivyokaa
vii. Kuangalia shingo ya kizazi, bartholin glands nk.
viii. Kuangalia sehemu ya haja kubwa kama kuna skin tags, bawasiri (haemorrhoids) nk.
ix. Kuangalia kwenye kinembe
kama kuna tatizo lolote lile.
kama kuna tatizo lolote lile.
Hayo
ni baadhi tu ya malengo na faida za kipimo hiki kwa vile humuwezesha
daktari kugundua tatizo au maradhi mengine ya ziada ambayo hayajaanza
bado kuonesha dalili zake kwa mgonjwa au mgonjwa mwenyewe hafahamu kama
hali aliyo nayo ni tatizo. Hata hivyo inashauriwa sana kabla ya kufanya
kipimo hiki, daktari amjulishe mgonjwa aina ya kipimo, lengo lake na
jinsi kitakavyofanyika ili kumuandaa mgonjwa kisaikolojia. Aidha ni
muhimu pia kumtaarifu wakati anapoanza kuingiza vidole.
2.
Kuchunguza uchafu unaotoka kwa kutumia hadubini (microscope). Mara tu
baada ya kuchukua sehemu ya uchafu kwa kutumia swab, kipimo hicho
humwagiwa tone la 10% potassium hydroxide ambayo huyeyusha chembechembe
za ngozi na kubakisha seli za Candida albicans. Kuwepo kwa pseudohyphae (mfano wa aina fulani ya mizizi au miguu ya fangasi hawa) pamoja na budding yeast cells (yaani seli za fangasi zinazojigawa kwa ajili ya kuzaliana) ni uthibitisho wa maambukizi ya fangasi aina ya Candida albicans.
3.
Kuchukua kipimo na kuotesha kwenye maabara ili kuangalia aina ya uoto
huo kama ni wa fangasi aina ya Candida albicans, ama la.
4. Kipimo cha mkojo (Urinalysis)
5.
Vipimo vingine hufanyika kulingana na dalili zinazoashiria uwepo wa
magonjwa mengine kama vile ugonjwa wa kisukari, HIV/AIDS, ugonjwa wa
kuvimba tezi la koo (goiter), saratani ya tezi koo (thyroid cancer) nk.
Matibabu
Matibabu ya fangasi huusisha dawa za kutibu fangasi (antifungal drugs) kama vile dawa za kupaka za topical Clotrimazole, topical Nystatin, Fluconazole au topical Ketoconazole.
Wagonjwa wenye maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated va#@ginal candidiasis wanaweza kutumia dawa za kupaka (cream) kutoka dawa za fangasi za jamii ya -azole kama vile Butoconozale, Miconazole, Clotricomazole
nk. Dawa hizi hutumika kwa muda wa siku 3-7 kulingana na aina ya dawa.
Mgonjwa anashauriwa kupaka dawa ndani ya uke pamoja na maeneo yote
yanayozunguka sehemu hiyo. Jinsi ya kupaka dawa hizi ni kuanzia mbele
kuelekea nyuma.
Aidha
mgonjwa anaweza kupewa dawa za kutumbukiza ukeni ambayo atatumia kwa
muda wa siku 3-14 kulingana na aina ya dawa. Dawa hizo ni pamoja na Miconazole, Tiaconazole, Terconazole, Nystatin nk. Kidonge cha kumeza aina ya fluconzole
pia huweza kutolewa. Dawa hizi nilizotaja hapa juu zina kawaida ya
kuharibu ubora wa mipira ya kondomu zilizotengenezwa na mpira aina ya latex (latex condoms)
pamoja na vifaa vya upangaji uzazi aina ya diaphragms. Ni vizuri kwa
daktari kabla ya kumpa mgonjwa dawa hizi kumfahamisha kwa ufasaha jinsi
ya kuzitumia na tahadhari anayotakiwa mgonjwa kuchukua. Inashauriwa
kama baada ya matumizi haya bado mgonjwa ana dalili za maambukizi au
mgonjwa akapata tena maambukizi haya ndani ya miezi miwili baada ya
matibabu ya awali, basi anashauriwa kwenda kumuona daktari ili apate
matibabu zaidi.
Kwa wale wenye maambukizi makali yaani complicated v@ginal candidiasis,
kabla ya kupewa tiba, ni muhimu kwanza kufanyiwa kipimo cha kuotesha
sehemu ya uchafu unaootoka ukeni ili kuwa na uhakika kama kweli fangasi
wanaosababisha maambukizi haya ni Candida albicans ama la, kwani fangasi aina ya Candida glabrata
pia wanaweza kusababisha aina ya maambukizi haya na huwa siyo rahisi
kutibika kwa kutumia matibabu ya kawaida ya kutibu fangasi pamoja na
pia si rahisi kuonekana kwa kutumia hadubini (microscope).
Matibabu
ya wagonjwa wenye aina hii ya fangasi hujumuisha matumizi ya dawa za
kupaka au vidonge vya kuweka ukeni kwa muda mrefu yaani kwa muda wa siku
saba hadi kumi na nne (7-14) au dawa aina ya fluconazole
ambayo hutumika kila baada ya siku tatu (yaani siku ya 1, siku ya 4 na
siku ya 7). Mara baada ya kumaliza tiba hii, mgonjwa hutakiwa kuendelea
nayo mara moja kwa wiki kwa muda wa miezi sita. Ikiwa matibabu haya
hayatasaidia basi mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia mchanganyiko wa
fluconazole pamoja na dawa ya kupaka ya Clotrimazole mara mbili au moja kwa wiki kulingana na dozi ya dawa, au fluconazole na dawa nyingine za kupaka kwa wakati mmoja.
Matibabu ya wagonjwa wenye maambukizi hatari sana yaani severe v@#ginal candidiasis
ambayo kwa kawaida huambatana na dalili kama uke kuwa mwekundu sana,
uke kuvimba, michubuko ya ngozi ya ukeni (excoriation) na kutokea kwa
mifereji kama vidonda (fissure formation) huwa ni dawa zozote za kupaka
zilizotajwa hapo juu kwa muda wa siku 7 mpaka 14 au dawa ya fluconazole
ambayo hutolewa mara mbili, ambapo dozi ya pili hutolewa siku ya tatu
baada ya kutolewa kwa dozi ya awali (second dose 72hrs after initial dose).
Matibabu ya maambukizi ya fangasi ambayo hayasababishwi na Candida albicans kwa mfano Candida glabrata nk ni matumizi ya dawa za kupaka jamii ya nonfluconazole azole groups kama vile Posaconazole, Voriconazole
nk zitolewazo kwa muda wa siku 7 mpaka 14 pamoja na kidonge cha Boric
acid kwa muda wa siku 14. Mtu mwenye maambukizi haya pia anashauriwa
kuonana na daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama.
Kwa
vile maambukizi ya fangasi hutokea sana kwa wanawake wajawazito, hivyo
basi wanashauriwa kutibiwa kwa kutumia dawa za kupaka tu kwa muda wa
siku 7. Aidha dawa aina ya Itraconazole haipaswi kutumiwa na mwanamke mjazito au anayekusudia kushika mimba. Dawa ya Ketoconazole haipaswi kutolewa bila ushauri wa daktari kwani ina madhara ya kusababisha ugonjwa hatari wa Ini (Fulminant hepatitis). Usugu wa fangasi dhidi ya dawa za jamii ya azole groups hutokea baada ya matumizi ya dawa za vidonge (vya kumeza) za kutibu fangasi kwa muda mrefu.
Maambukizi
ya fangasi pia huonekana sana kwa wagonjwa wenye Ukimwi. Tiba ya
maambukizi haya ni sawa na tiba ya watu ambao hawana ugonjwa wa Ukimwi.
Hata hivyo, kwa wale wagonjwa wa ukimwi ambao wamepata maambukizi ya
fangasi mara kwa mara wanashauriwa kunywa dawa aina ya fluconzole mara
moja kwa wiki kama kinga dhidi ya maambukizi haya au kama njia ya
kupunguza fangasi hawa. Kadhalika dawa za kutibu fangasi aina ya Itraconazole, Voriconazole, Posaconazole
huingiliana sana katika utendaji kazi na dawa za kurefusha maisha za
ugonjwa wa Ukimwi (Antiretroviral drugs, ARVs) aina ya Protease
Inhibitors, PIs (rotinavir nk.) na Nonnucleoside Reverse Trancriptase
Inhibitors, NNRTI (maraviroc nk).
Wakati mwingine, maambukizi ya fangasi yanaweza kuambatana na magonjwa ya zinaa (Bacterial vaginosis nk), hivyo dawa zitatolewa kulingana na dalili na historia ya mgonjwa.
Kinga ya maambukizi ya fangasi
•
Kuosha sehemu ya siri kwa kutumia kitambaa kisafi kila siku na kuosha
kuanzia mbele kuelekea nyuma, epuka kurudia ukishafika nyuma.
• Epuka matumizi ya sabuni zenye manukato, bubble baths, v@#ginal deodorant products, feminine hygiene, na bath powder.
• Vaa chupi ambazo hazibani sana na zilizotengenezwa kwa kutumia pamba au hariri (silk), epuka synthetic underwear.
• Epuka mavazi yoyote ya kubana kama jeans za kubana nk.
• Badilisha nguo za ndani (chupi) kila zinapopata unyevunyevu.
• Fua chupi zako kwa maji yenye nyuzi joto 90 na kuendelea.
• Tumia pad wakati tu unapozihitaji (kama umeingia kwenye mzunguko wako wa hedhi)
• Kula mlo wenye virutubisho vyote kamili (balanced diet)
• Epuka kufanya mapenzi na mpenzi wako ambaye amepata maambukizi ya fangasi.
•
Epuka kuoga maji moto sana (hot baths) tumia maji ya uvuguvugu, hii
kwa wale ambao wanaishi kwenye ukanda wa joto (tropical climate).
•
Matumizi ya vifaa vya ngono , vifaa vya upangaji uzazi (diaphragms,
cervical caps) yanaweza kuleta kujirudia kwa maambukizi ya fangasi kama
havitaoshwa na kukaushwa vizuri baada ya kutumiwa.
•
Baadhi ya tafiti zilizofanyika, zimethibitisha ya kwamba unywaji wa
maziwa ya mtindi (yoghurt) yenye live culture, husaidia kupunguza
maambukizi ya fangasi
0 MAONI :
Post a Comment