![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgUZV72NApZMt2a5jZ6gXLS9Nr39UlrbzHnQtoYdvJb3TqygObN3mHmwv0l2VfoN8Y4BFxtAZf-3Q7YsuIKti3RztDhTH7iBDS43cuvU71uK6yhK1JYd_zrL7gXr3iqPHL3jRHwRANoB3Ch/s1600/John-Kerry-speaking-in-Lo-016.jpg)
Baada ya mashambulizi ya vikosi vya Marekani nchini Libya na Somalia ambayo yalisababisha kukamatwa mtuhumiwa anayesakwa kwa kuhusika na ulipuaji wa balozi za Marekani barani Afrika miaka 15 iliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amewaonya wanamgambo wa kigaidi wa al-Qaeda kuwa wanaweza kukimbia lakini hawataweza kujificha. Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema Nazih al-Ragye, anayefahamika kwa jina la Abu Anas al-Liby, alikamatwa na majeshi ya Marekani katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, hapo jana. Shambulizi lililofanywa katika mji wa bandari kusini mwa Somalia wa Barawe, ambao ni ngome ya kundi la al-Shabaab lililohusika na shambulizi la mwezi uliopita katika jumba la kibiashara la Westgate jijini Nairobi, nchini Kenya, lilishindwa kumpata mtuhumiwa mkuu. Waziri Kerry amesema leo kuwa huu ni ujumbe wa wazi kuwa Marekani haitasitisha juhudi zake za kuwasaka watuhumiwa wa ugaidi. Liby, raia wa Libya anayeaminika kuwa na umri wa miaka 49, amekuwa akisakwa na Marekani kwa madai ya kuhusika na milipuko ya mwaka wa 1998 katika balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania, ambayo iliwauwa watu 224.
0 MAONI :
Post a Comment