Shirikisho liko kwenye hatua za mwisho za mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 26/27 Oktoba 2013 hapa jijini Dar es salaam.
Hivi
sasa, wagombea wanasubiri vyombo vya juu vya uamuzi kwa ajili ya kutoa uamuzi wa
mwisho kabla ya kuanza kampeni na hatimaye uchaguzi.
Hata
hivyo, baada ya Kamati ya Maadili kufanya uamuzi dhidi ya kesi nane
zilizowasilishwa mbele yake, Sekretarieti imeona kuwepo kwa ukakasi katika
utekelezaji wa uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa kuna baadhi ya mambo
yanaonekana kuwa na ugumu katika kuyatekeleza.
Sekretarieti
si chombo chenya mamlaka ya kutafsiri uamuzi wa vyombo huru vya Shirikisho, kazi
yake kubwa ni kupokea uamuzi na kuutekeleza, hivyo kwa kuwa kuna ukakasi huo imeamua
kuwasilisha uamuzi huo kwenye Kamati ya Rufani ya Maadili kwa ajili ya kuufanyia
mapitio (revision) na pia kutoa mwongozo kabla ya kurejesha uamuzi huo kwenye
Kamati ya Uchaguzi kwa ajili ya kuendelea na mchakato.
Sekretarieti
imefanya hivyo kwa lengo la kusaidia wagombea ambao wengi wanaonekana kuwa njia
panda baada ya kupokea uamuzi wa Kamati ya Maadili na kuiuliza Sekretarieti
kuwa inakuwaje Kamati ya Maadili iwaone hawana hatia, lakini hapo hapo
ikubaliane na uamuzi wa kuwaengua, jambo ambalo kwa kweli limetufanya tukose
majibu sahihi na hivyo kuamua kuomba revision na mwongozo.
Pia
mwongozo utakaotolewa na Kamati ya Rufani ya Maadili utasaidia kuweka mwelekeo
mzuri wa masuala ya Maadili katika siku zijazo.
Miongoni
mwa mambo yanayoonekana kuwa na ukakasi ni kuwaona watu wote ambao kesi zao
ziliwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili hawana hatia, lakini hapo hapo
kukubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi wa kuwaengua baadhi yao kwa sababu
za kinidhamu ikisema haiwezi kuwahukumu mara mbili kwa kuwa wameshaadhibiwa kwa
kuenguliwa kwenye uchaguzi.
Ili
haki itendeke na ionekane inatendeka, Sekretarieti imeona ni vizuri masuala
hayo yakafanyiwa revision (mapitio) na kutolewa mwongozo ili kuondoa ukakasi
uliojitokeza miongoni mwa wagombea, Shirikisho na wadau na hivyo kujenga hisia
kuwa kuna mbinu zimefanyika dhidi ya baadhi ya wagombea.
Uamuzi
huu haumaaniishi kuwa Sekretarieti inapingana na uamuzi wa Kamati ya Maadili,
bali ni utaratibu wa Sekretarieti kuomba ufafanuzi au mwongozo kutoka vyombo
husika pindi inapotokea ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi wa vyombo vya uamuzi
vya Shirikisho.
Sekretarieti
imeshamwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani za Maadili ili aitishe kikao kwa
manajiri ya kufanya mapitio na kutoa mwongozo ambao utasaidia Shirikisho
kuendelea na uchaguzi bila ya ukakasi.
SERIKALI, TAASISI ZAOMBWA KUISAIDIA U20 WANAWAKE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limeiomba Serikali, taasisi na kampuni mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa
ya mpira wa miguu ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20
inayojiwinda kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji.
Timu hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi
mkoani Pwani chini ya Kocha Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza
ya raundi ya kwanza itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya
Wanawake ya TFF, Lina Kessy amesema hiki ndio kipindi muafaka cha kuisaidia
timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Ameitaka jamii kujitokeza kuisaidia timu
hiyo ambayo haina mdhamini wala mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania
badala ya kusubiri ifanye vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.
Kessy ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama
cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu
kwa kutoa fursa ya kambi kwani timu hiyo hailipii malazi badala yake inalipia
huduma nyingine inazopata hapo.
Vilevile amewashukuru wadau mbalimbali
ambao wamekuwa wakijitolea kutokana na ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya
mpira wa miguu wa wanawake kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.
“Shukrani za kipekee kwa wazazi kukubali
watoto wao wachezee timu ya Taifa, kwani wengi bado wanasoma na wapo chini ya
uangalizi wa wazazi. Pia tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga
kisaikolojia wachezaji wetu,” amesema.
Fainali za Dunia za U 20 kwa wanawake
zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo Tanzania itaitoa Msumbiji katika
raundi hiyo, raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana na
Zimbabwe.
0 MAONI :
Post a Comment