Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kupitia Jeshi la Polisi kuanzia sasa halitashikilia silaha za washabiki,
na badala yake litawazuia kabisa kuingia viwanjani wakati wa mechi.
Jeshi la Polisi limekuwa likihifadhi
silaha za washabiki wanaokwenda viwanjani, na baadaye kuwarejeshea baada ya
mechi kumalizika kwa vile Kanuni za Usalama Viwanjani za Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zinakataza silaha viwanjani.
Wikiendi iliyopita katika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi lilikamata bastola 17 katika upekuzi wa
washabiki waliokwenda kushuhudia mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ile
kati ya JKT Ruvu na Simba. Wote waliokutwa na silaha hizo walikuwa na leseni za
kuzimiliki.
Hivyo, kwa washabiki wanaomiliki silaha
hatawaruhusiwa kabisa kuingia viwanjani, na badala yake tunawashauri
kuzihifadhi huko wanakotoka kabla ya kufika viwanjani.
Pia tunatoa mwito kwa shabiki ambaye
atamuona mwenzake akiwa na silaha uwanja kutoa taarifa kwa mamlaka husika
likiwemo Jeshi la Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua.
SIMBA KUIVAA RUVU SHOOTING VPL
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya saba kesho (Oktoba 5 mwaka
huu) kwa mechi nne ambapo Ruvu Shooting
itakuwa mwenyeji wa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio katika mechi hiyo
itakayochezeshwa na mwamuzi Mohamed Theofil kutoka Morogoro kuanzia saa 10
kamili jioni vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Tiketi
zitauzwa uwanjani kuanzia saa 4 asubuhi.
Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu
itakayoumana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku
Coastal Union ikiwa mwenyeji wa Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta
Amri Abeid jijini Arusha ndiyo utakaotoa fursa kwa timu za Oljoro JKT na Mbeya
City kuoneshana ujuzi katika kusaka pointi tatu.
Ligi hiyo itaendelea Jumapili (Oktoba 6
mwaka huu) kwa mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam wakati Mgambo Shooting itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa
Mkwakwani jijini Tanga.
FDL KUTIMUA VUMBI VIWANJA KUMI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania
tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2014/2015) inaendelea
wikiendi hii (Jumamosi na Jumapili) kwa kuzikutanisha timu 20 zitakazopambana
katika viwanja kumi tofauti.
Jumamosi kutakuwa na mechi kati ya Green
Warriors na Friends Rangers (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Kimondo na Burkina
Faso (Uwanja wa CCM Vwawa, Mbozi), Mlale JKT na Mkamba Rangers (Uwanja wa
Majimaji, Songea) na Kurugenzi dhidi ya Polisi Morogoro (Uwanja wa Wambi,
Mafinga).
Polisi Dodoma na Stand United (Uwanja wa
Jamhuri, Dodoma), Toto Africans na JKT Kanembwa (Uwanja wa CCM Kirumba,
Mwanza), Mwadui na Polisi Mara (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) na Polisi
Tabora na Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi
kati ya African Lyon na Transit Camp (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Villa
Squad dhidi ya Polisi Dar es Salaam (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam).
Idara ya Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 MAONI :
Post a Comment