Tangaza na Abd Da Hustler

Kagame ahimizwa kuwa mvumilivu na Umoja wa Mataifa


Wanajshi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito kwa rais wa Rwanda, kuwa mvumilivu huku uhasama kati yake na nchi jirani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ukiendelea kutokota katika maeneo ya mipakani.
Bwana Ban, alizungumza na rais Paul Kagame baada ya serikali yake kuishutumu Congo, kwa kufanya shambulio katika ardhi yake makusudi na kumuua mama mmoja na kumjeruhi mtoto wake.
Msaidizi wa katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa, amenukuliwa akiiambia Umoja wa Mataifa kuwa wapiganaji wa kundi la waasi wa M23, wameonekana wakirusha makombora wakilenga Rwanda.
Serikali ya DRC na Umoja wa Mataifa zimeshutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao wa M23, madai ambayo yamepingwa vikali ya utawala wa Kigali.
Wanajeshi wa Congo wakishirikiana na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, wamekuwa wakifanya mashambulio dhidi ya waasi hao wa M23 karibu na mpaka wa Rwanda, tangu wiki iliyopita.

Waasi walengwa na UN

Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kutunza amani nchini DRC, Monusco, kiliimarishwa zaidi pale wanajeshi elfu tatu zaidi walipotumwa nchini humo kupambana na waasi hao.
Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo, amesema mabomu na makombora kumi na tatu yalirushwa katika ardhi yake siku ya Jumatano na mengine kumi siku ya Alhamisi.
Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
Waziri huyo amedai kuwa kufikia sasa wanajeshi hao wa Congo wamefanya mashambulio thelathini na nne nchini Rwanda.
Amewashutumu wanajeshi wa DRC kwa kuwalenga raia wake na kusisitiza kuwa kwa sasa wanajiepusha kulipisa kisasi lakini hawatasita kujibu ikiwa uchokozi huo hautakoma.
Msemaji wa jeshi la Congo Kanali Olivier Hamuli ameiambia BBC kuwa jeshi lake haliwezi kurusha makombora kulenga maeneo yanayokaliwa na raia.
''Waasi ndio wanaoweza kufanya kitendo kama hicho, wapiganaji wa M23 na wala sio wanajeshi wake ndio waliokuwa katika eneo ambalo makombora hayo yalirushwa'' Alisema Kanali Hamuli.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Mulet ambaye aliiambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, wanajeshi wake nchini DRC walishuhudia wapiganaji wa M23, wakirusha makombora wakilenga Rwanda na wala sio wanajeshi wa Congo.
Takriban watu laki nane wamekimbia makwaoi nchini Congo tangu waasi hao wa M23 kuanzisha mashambulio katika eneo la Mashariki mwa Congo Aprili mwaka wa 2012
Share on Google Plus

About Unknown

Naitwa Abdalla Ngowi, Napenda Michezo na kukupa habari mbalimbali kutoka katika kila kona ya ulimwengu huu!, karibu ABD da Hustler
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 MAONI :

Post a Comment